Na George Binagi-GB Pazzo wa BMGHabari.com
Waandishi wa Habari za Madini Kanda ya Ziwa wamejizatiti kuandika zaidi habari na makala kuhusiana na sekta hiyo ili kuibua masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Wakizungumza jana Jijini Mwanza kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yao walioifanya kwa siku mbili kuanzia Julai 03,2017 mkoani Geita, waandishi hao walisema bado sekta ya madini kama zilivyo sekta nyingine asilia hapa nchini, inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji kwenye sekta hiyo.
“Ukiangalia maeneo niliyotembelea mkoani Geita ikiwemo Nyamalembo ambako kuna bwawa linalodaiwa kuwa na maji yenye sumu, bado hakuna ukweli kwa wananchi ama mamlaka husika kuhusiana na bwawa hilo jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za wananchi ambao wanadaiwa kutumia maji hayo”. Alisema Malongo Mbeho, mmoja wa waandishi hao.
Kwa ujumla waandishi hao walisema katika maeneo mengi yenye raslimali madini ikiwemo Geita, huduma za kijamii kama vile maji, afya, barabara ikiwa ni miongoni mwa huduma msingi nyingi siyo rafiki na hivyo kuahidi kutumia kalamu na kamera zao vyema katika kuibua changamoto hizo.
Waandishi hao walianza kuiangazia sekta ya madini baada ya kupokea mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwa Shirika la Demokrasia na Utwala Bora nchini ADLG lenye makazi yake Jijini Mwanza ambalo limekuwa likiwajengea uwezo wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wananchi na viongozi wa serikali za mitaa ili kutambua mchango wa raslimali asilia ikiwemo madini kwa ajili ya maendeleo ya jamii husika.
Waandishi wa Habari za Madini Kanda ya Ziwa
Tazama HAPA video