DC IKUNGI AIONYA BODI YA CHAMA CHA USHIRIKA AMINIKA KWA KUSHINDWA KUWAJIBIKA

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Mhe.Miraji Mtaturu ametoa onyo kali kwa bodi ya uongozi wa Chama cha Ushirika cha wachimbaji wadogo wa dhahabu cha Aminika kilichopo kijiji cha Mang’onyi wilayani humo kutokana na kuendesha chama hicho kiholela.

Mhe.Mtaturu alitoa onyo hilo jana Agosti 18,2017, alipokutana na wanachama pamoja na uongozi wa chama hicho kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wanachama.

Awali Katibu wa chama hicho, Ally Nkingi alisema baada ya chama kupokea fedha hizo kilinunua mashine (compressor) kwa ajili ya shughuli za uchimbaji iliyogharimu zaidi ya shilingi Milioni 30, milioni 41 zikalipa madeni, milioni kumi zikatumika kulipia leseni ya uchimbaji na milioni 15 zikatumika kwa ajili ya ununuzi wa mafuta, baruti, kusafirisha mashine kutoka Dar es salaam na uendeshaji wa kambi.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho walieleza kwamba hawajawahi kusomewa mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba hawajui pesa walizosaidiwa na serikali pamoja na mwekezaji kutoka kampuni ya Shanta Gold Mining zimefanya kazi gani.

“Miaka mitatu hatujawahi kukaa na bodi yetu kuelezwa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zetu. Tunasikia tu imenunuliwa mashine (Compressor) lakini sisi hatujawahi kuiona na tunaambiwa huwa inakodishwa lakini fedha zake hatuzioni, tukiwauliza viongozi wanakuwa wakali”. Alieleza Bi.Patrice Petro.

Wanachama wengine ambao ni pamoja na mzee Masoud Hassan, Florentina Yohana na Anna Petro walisema uongozi uliopo madarakani unawapeleka shimoni kwani maisha yao ya uchimbaji yamekuwa magumu kutokana na kukosa vifaa kwa ajili ya uchimbaji hivyo wanaomba serikali iwasaidie wapate ripoti ya utafiti wa madini katika eneo la Mang’onyi kwa ajili ya kuingia makubaliano na mwekezaji ambaye alisema baada ya ripoti hiyo kutoka na kubaini kiwango cha dhahabu kilichopo atatoa vifaa kwa ajili ya uchimbaji na faida itakayopatikana watagawana.

Baada ya maelezo hayo, Mhe.Mtaturu alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati, Sosthenes Massola kuhakikisha ripoti hiyo inapatikana katika kipindi kisichozidi wiki mbili huku akimtaka Afisa Ushirika Gurisha Msemo kuhakikisha anasimamia vyema ushirika huo ikiwemo kufanya uchaguzi wa uongozi kwani kwa mjibu wa katiba, muda wa ushirika huo kufanya uchaguzi umewadia.

Mwenyekiti wa bodi ya Chama cha Ushirika Aminika Mang’oni, Francis Mbassa awali hakuwa wazi kukiri malalamiko juu ya uongozi wake na baada ya DC Mtaturu kumuonya kuacha tabia hiyo akakiri kuwepo kwa baadhi ya mapungufu ya kiuongozi na kuahidi kumaliza mvutano uliopo ikiwemo kuitisha mkutano wa wanachama kwa ajili ya uchaguzi kwani muda wa uongozi uliopo madarakani umekwisha.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Miraji Mtaturu akizungumza kwenye mkutano huo
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Miraji Mtaturu akizungumza kwenye mkutano huo